Charles Mwijage Waziri wa Viwanda na Biashara
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage ametoa takwimu hizo leo jijini Dar es Salaam wakati akitangaza kuanza kwa maonesho ya kwanza ya viwanda vya Tanzania yatakayofanyika kuanzia tarehe 7 hadi 11 Desemba mwaka huu.
“Maonesho hayo yatafanyika katika uwanja wa maonesho wa Mwalimu Nyerere maarufu kama Sabasaba maeneo ya barabara ya Kilwa Jijini Dar es Salaam, kauli mbiu yake ikiwa ni 'Tanzania sasa Tunajenga Viwanda,” alisema Mhe. Mwijage.
Waziri Mwijage amesema, maonesho hayo yanalenga kuwapa fursa wazalishaji wa viwanda nchini kutangaza fursa zilizopo katika sekta hiyo sambamba na kujadili changamoto zinazoikumba sekta hiyo hasa ubora wa bidhaa.
Maonesho hayo yatajumuisha wazalishaji wa malighafi, taasisi zinazotoa huduma kwa wenye viwanda, wasafirishaji wa bidhaa ambapo Wizara ya Viwanda imeandaa maonesho hayo kupitia taasisi yake ya Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara ya Tanzania (TanTrade).

