Jumatatu , 13th Feb , 2017

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nape Nnauye amefunguka na kusema kuwa watu wote tunatakiwa kuungana kupambana vita dhidi ya dawa za kulevya ila vita hiyo inapswa kufanywa kwa kutenda haki na kusimamia haki na si kuwaonea watu.

Nape Nnauye

Waziri Nape amesema hayo katika maadhimisho ya 'Siku ya Radio Duniani' na kuwataka waandishi wa habari kwa pamoja kuungana katika kuunganisha taifa la Tanzania.

"Kulikuwa na mjadala mkubwa wa madawa ya kulevya, wito wangu kwa wana habari tuliunganishe taifa letu kuwa kitu kimoja kwa kuungana pamoja katika kupiga vita dhidi ya madawa ya kulevya hili ndiyo kubwa sana, tuna vita dhidi ya madawa ya kulevya vyombo vyetu vyote viungane pamoja, tasnia zote ninazoongoza lazima zipige vita hii kwa sababu kushinda ni lazima na Rais ametuelekeza tupambane na madawa ya kulevya" alisema Nape Nnauye 

Waziri Nape Nnauye amesisitiza katika vita hii dhidi ya madawa ya kulevya haipaswi kuwa vita yenye kuonea mtu bali haki itendwe

"Niwaombe wana habari sisi tuna uwezo wa kuunganisha taifa letu likapambana katika vita hii ya dawa za kulevya, kwa sababu athari zake ni kubwa kwa hiyo naomba kutumia siku hii ya radio duniani kutoa wito na ombi langu kwenu wana habari na kwa wote ambao wako chini ya wizara yangu, wanamichezo, wanahabari, wana utamaduni na wasanii tuungane kwa pamoja tumuunge mkono Rais na wote wanaopambana katika vita hii ya madawa ya kulevya". Alimalizia Waziri Nape Nnauye