Ijumaa , 13th Mar , 2015

Viongozi watatu wa chama cha Demkrasia na Maendeleo CHADEMA wamefunguliwa mashitaka kwa kuhusika na tukio la kumshikilia aliyekuwa mlinzi wa Dkt Wilbroad Slaa isivyo halali.

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, leo limetoa ufafanuzi kuhusiana na mahojiano iliyoyafanya hapo jana na katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema Dkt Wilbrod Slaa, kuhusiana na njama za kuuwawa kwa sumu kutoka kwa aliyekuwa mlinzi wake Bw. Khalid Kagenzi.

Akizungumza na waandishi wa habari katika makao makuu ya kanda hiyo, Kamishna wa polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleima Kova amesema kimsingi wamebaini kuwepo kwa mashauri mawili ambayo yote wameshafungua kesi katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Kamishna Kova ametaja mashauri hayo kuwa ni lile la Tishio la Kudhuru Maisha na Uhai wa Dkt Slaa na la pili ni la madai ya kuteswa pamoja na kushikiliwa isivyo halali kwa Bw. Kagenzi, ambapo baadhi ya maofisa wa idara ya ulinzi na usalama ya CHADEMA wanatuhumiwa kuyafanya.

Wakati huo huo Jeshi la Polisi limemtia mbaroni bwana Haroub Mtopa 44 mkazi wa maeneo ya Mbagala Rangi Tatu kwa tuhuma za kujipatia fedha kwa kupitia ofisi ya Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.