Jumanne , 8th Sep , 2015

Viongozi wa dini mkoa wa Arusha wamewataka watanzania kuungana pamoja katika kuilinda na kuitunza amani iliyopo pasipo kujali itikadi za vyama, udini, ukabila na ukanda kwa kuwa iwapo itapotea ni vigumu kuirejesha.

Thomas Godda-mkurugenzi taasisi ya amani Tanzania

Wakizungumza katika kongamano la amani lililowakutanisha viongozi wa dini kutoa madhehebu mbalimbali mkoani humo wamesema kila mtanzania anao wajibu binafsi kuhakikisha hadhuru wala kuingilia amani na uhuru wa mwenzake, katika kipindi hiki cha uchaguzi.

Kwa upande wake mwakilishi wa kamanda wa polisi mkoa wa Arusha Liberatus Sabas, Yona Masimba amewataka wananchi kuwa na imani na jeshi la polisi kwa kuwa linaongozwa kwa sheria na kanuni.

Aidha Masimba pia amewakumbusha wakazi wa mkoa wa Arusha kuwa makini na kauli za uchochezi zinazotolewa na baadhi ya wanasiasa kwa kuwa zinaweza kuwapeleka katika uvunjifu wa amani.

Kongamano hili limewakutanisha zaidi ya viongozi mia mbili kutoka katika taasisi mbalimbali za dini ikiwa ni sehemu ya jitihada vinazofanywa na kamati ya mahusiano ,upendo na amani mkoa wa Arusha ya kuboresha amani.