Alhamisi , 19th Mar , 2015

Kamati ya amani ya Madhehebu ya dini Mkoa wa Dar es Salaam imemtaka Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi CCM, Bw. Abdulrahman Kinana, kuwa makini na kauli anazozitoa dhidi ya viongozi na watendaji wa serikali, hususani wale wanaolalamikiwa na wananchi.

Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Sheikh Mkuu Mkoa wa Dar es Salaam , Alhad Mussa Salum amesema hayo leo kufuatia kile alichodai kuwa ni kauli za kukatisha tamaa ambazo Katibu Mkuu huyo wa CCM amekuwa akizitoa kwenye ziara anazofanya katika maeneo mbalimbali nchini hivi sasa, na badala yake ajikite katika kuzungumzia namna ya kutatua mahitaji ya msingi ya wananchi.

Sheikh Salum ametaja moja ya kauli zilizotolewa na Kinana kuwa ni pamoja na ile aliyomtuhumu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu kuwa amekuwa ni mtu wa kupenda kusafiri pasipo kushughulikia kero za wananchi.

Kwa mujibu wa Sheikh Salum, kauli kama hiyo ni ya kukatisha tamaa kwa viongozi wachapakazi kama waziri Nyalandu, ambaye kwa muda mrefu amekuwa akionesha uzalendo kwa taifa lake kwa jinsi anavyoshughulikia tatizo la ujangili na uwindaji haramu.

Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Amani ya Madhehebu ya Dini mkoa wa Dar es Salaam, amesema viongozi kama waziri Nyalandu wanapaswa kuungwa mkono na kupongezwa kwa jinsi wanavyochapa kazi badala ya kuonekana kuwa ni kikwazo kwa maendeleo.

Aidha, akizungumzia mchakato wa kura ya maoni ya Katiba Inayopendekezwa, Shekh Salum amesema Waislam wana wajibu wa kuisoma katiba hiyo na kuielewa vizuri ifikapo April 30 wakati wa kupiga kura ya maoni, wafanye maamuzi sahihi pasipo kushinikizwa na mtu yoyote.