Ijumaa , 12th Feb , 2016

TAKUKURU yawafikisha mahakamani viongozi 11 wa shirika la Reli Tanzania TRL ,kwa tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka.

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini Tanzania TAKUKURU imewafikisha katika mahakama ya hakimu mkazi kisutu jijini Dar es salaam viongozi 11 wa Shirika la Reli Tanzania TRL, wakituhumiwa kutumia madaraka yao vibaya kwa kuingiza mabehewa 25 nchini yaliyo chini ya kiwango na kuisababishia hasara serikali.

Watuhumiwa hao 11 ikiwa ni pamoja na mkurugenzi mkuu,mhandsi mkuu pamoja na mhandisi mwandamizi wa mitambo wa shirika hilo wamefikishwa mahakamani wakituhumiwa kuwezesha kufanikisha kupitisha zabuni iliyotajwa kuwa ni PA/113/2012-13/ME/G/OE/013 ya ununuzi wa mabehewa 25 ya mizigo kinyume na kanuni na taratibu chini ya sheria ya ununuzi wa umma ya mwaka 2004 zilizotumika katika ununuzi huo.

Akiwasomea mashtaka yao, mwendesha mashtaka wa TAKUKURU Max Ali mbele ya hakimu mkazi mkuu Emilius Mchauru amesema watuhumiwa hao 11 wanakabiliwa na mashtaka tisa tofauti ambapo inadaiwa kuwa kati ya Januari 1 na Februari 28 mwaka huu makao makuu ya Shirika la Reli Tanzania miongoni mwao viongozi hao wa shirika walitumia madaraka yao kuidhinisha ununuzi wa mabehewa 25 yaliyokuwa chini ya kiwango.

Viongozi hao wa juu wa shirika waliingia mkataba na kampuni ya Hindusthan Engineering and Industries Limited ya India bila kujiridhisha kuhusu uwezo wa kampuni hiyo kama ilivyoelekezwa kwenye nyaraka za zabuni.

Watuhumiwa hao 11 wanakabiliwa na mashtaka 9 ikiwa ni pamoja na kuidhinisha kulipwa kwa dola 1,280,593, za kimarekani kutoa taarifa za kupotosha ukweli zinazodai kuwa mabehewa hayo 25 yamekaguliwa, kuidhinisha kampuni hiyo kutengeneza mabehewa hayo 25.

Watuhumiwa hao ili kupata dhamana wametakiwa kulipa dhamana ya shilingi milioni 10 pamoja na kuwa na wadhamini watatu wanaofanya kazi zinazotambulika pamoja na kutoa hati zao za kusafiria na hawaruhusiwi kusafiri kwenda nje ya mkoa wa Dar es salaam pasipo kuwa na kibali cha mahakama, kesi hiyo itaanza kusikilizwa Feb 25 mwaka huu.