Jumatano , 11th Oct , 2023

Naibu Waziri wa Uchukuzi David Kihenzile amesema Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere - Terminal 2 unatarajia kufanyiwa maboresho makubwa mwaka 2024 ambapo yatapelekea kufungwa kwa muda kwa uwanja huo ili kufanya maboresho hayo.

Terminal 2

Kihenzile ameyasema hayo alipokuwa Jijini Dar es Salaam wakati akiendelea na ziara yake ya siku mbili ya kukagua kwa lengo la kujuonea namna shughuli zinavyoendela katika uwanja huo.

Kihenzile amesema endapo wananchi wataona uwanja huo umefungwa kwa muda mwakani wasishtushwe au kupotoshwa wajue kuwa ni ukarabati huo umeanza na utakamilika kwa haraka ili shughuli zake ziendelee.

Kihenzile amesema maboresho hayo ni kutokana na juhudi za Serikali za kuuongezea uwanja huo uwezo wa kuhudumia abiria wengi zaidi kwani jitihada za  Rais Dkt. Samia suluhu Hassan za kuitangaza Nchi kupitia filamu ya Tanzania The Royal Tour zimezaa matunda yanayopelekea uhitaji wa kupanua uwanja hio kutokana na ujio wa Wageni wengi.

Katika hatua nyingine  Kihenzile amesema ameridhishwa na jitihada zinazofanya na Uongozi wa Uwanja huo za kuhakikisha usalama wa ndege na abiria  na kusisitiza kuwa katika jambo muhimu kwenye uwanja wa ndege ni usalama wa abiria, mizigo yao na ndege yenyewe.