Jumapili , 31st Jul , 2016

Uongozi wa jiji la Dar es salaam umetakiwa kuendeleza juhudi za kuimarisha hali ya usafi na utunzwaji wa mazingira sambamba na kuifanya jiji la Dar es salaam kuwa na muonekano wa kibiashara na kivutio kwa wageni.

Ushauri huo umetolewa jijini Dar es salaam na mtendaji mkuu wa Hoteli ya Kimataifa ya Dar es Salaam Serena Hotel Bw. Rahim Azad alipokuwa akiongea na East Africa Radio wakati wa zoezi la usafi kwenye maeneo yanayozunguka Hoteli hiyo.

Rahim Azad amesema, jitihada zinazo fanywa hivi sasa za kubadilisha muonekano wa jiji la Dar es salaam uende sambamba na uwekezaji wa majengo ya kisasa huku akiwataka wawekezaji kujikita katika ujenzi wa miundombinu inayotunza mazingira.

“Wawekezaji wa Hoteli na majengo makubwa wanawajibu mkubwa ya kuhakikisha jiji la Dar es salaam linakuwa safi na muonekano mzuri, hivyo Dar es salaam Serena Hotel inaunga mkono juhudi za jiji na tamko la Rais la kuhakikisha mazingira yanayozunguka maeneo yetu ni masafi na salama”

Aidha Rahim amesema, endapo uhifadhi wa vivutio vya kitalii vilivyopo ndani ya jiji la Dar es salaam akitolea mfano fukwe za bahari zitaifadhiwa ipasavyo na kutangazwa kimataifa ni njia nzuri ya kuongeza makusanyo ya kodi kwa serikali na kuongeza kipato kwa wafanyabiashara wawekezaji.

Mbali na kudumisha hali ya usafi uongozi wa jiji pia umetakiwa kuhakikisha hali ya usalama inaendelea kuimarishwa kwani usalama ni miongoni mwa kivutio kwa wageni huku akiwataka wananchi kujenga tabia ya kutunza mazingira kwa kuacha kutupa taka ovyo katika maeneo yao.