Jumatatu , 13th Jun , 2016

Serikali imesema imetenga fedha kiasi cha shilingi milioni 430 kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina katika barabara ya Tarime kwenda Nyamwaga hadi Mugumu katika mwaka wa fedha 2016 & 2017.

Hayo yamesemwa Bungeni Dodoma na Naibu Waziri wa Ujenzi Mhandisi Edwin Ngonyani wakati akijibu swali la Mbunge wa Tarime Vijijini John Heche kuhusu ujenzi wa barabara hiyo ambayo ni kiungo cha biashara ya utalii wa kwenda mbuga Serengeti na kichocheo ya maendeleo kwa mkoa wa Mara.

Naibu Waziri Ngonyani amesema kwamba serikali imeendelea kujenga barabara za mkoa wa Mara ambapo kilomita 6 kutoka Tarime kwenda Mugumu zimekamilika na kuahidi kuendelea kumalizia barabara nyingine.

Aidha Naibu Waziri amesema serikali pia imetenga bilioni 1 kwa ajili ya ujenzi wa daraja la Mara ili kuweza kufanya Barbara hizo kuweza kupitika vizuri pia upembuzi yakinifu ukikamilika serikali itaanza kutafuta fedha za ujenzi wa barabara hizo kwa kiwango cha lami.