Jumatatu , 7th Dec , 2015

Jumla ya tani 4,000 za korosho zimekusanywa na Chama Kikuu cha Ushirika cha MAMCU kutoka kwa wanunuzi holela wa zao hilo (Kangomba), kufuatia jitihada zinazofanywa na bodi ya korosho Tanzania za kudhibiti ununuzi huo katika maeneo mbalimbali.

Kaimu Meneja mkuu wa Chama Kikuu cha Ushirika cha MAMCU, Kalvin Rajab

Akizungumza mkoani Mtwara, Kaimu meneja mkuu wa chama hicho, Kalvin Rajabu, amesema, kumekuwa na jitihada za dhati zinazofanywa na bodi kuhakikisha wanatokomeza ulanguzi huo ambao umekithiri katika maeneo ya vijijini na kwamba jitihada hizo zinaonesha kufanikiwa.

Amesema kuwa baada ya bodi ya kurosho kufanya kazi yao vizuri bodi imeweza kupata zaidi ya wastani wa tani 4000 ambazo zimerejeshwa kutoka kwa wanunuzi wanaotumia mfumo ambayo sio halali.

Aidha, amesema, hali ya mauzo kwanzia mwezi Septemba ulivyozinduliwa na bodi, inaenda vizuri na kwamba mpaka kufikia Novemba 27 mwaka huu chama hicho tayari kimeshafanya minada saba ambapo jumla ya tani 30,588 ziliingizwa sokoni na kuuzwa.