Alhamisi , 26th Mei , 2016

Ukuaji wa sekta ya viwanda nchini Tanzania hivi sasa umefikia asilimia saba kwa mwaka huku ikichangia wastani wa asilimia saba ya pato lote la taifa.

Aidha, sekta hiyo pia ni moja ya sekta chache zinazosaidia kupunguza tatizo la ajira kwa kuchangia asilimia kumi na moja ya ajira zote rasmi zinazopatikana nchini hivi sasa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirikisho la Wenye Viwanda nchini CTI, Bw. Leodgar Tenga, ametoa takwimu hizo jijini Dar es Salaam leo wakati akizungumzia Tuzo ya Rais ya Mzalishaji Bora nchini itakayotolewa Mei 31 mwaka huu ambapo rais John Pombe Magufuli ndio mgeni rasmi katika hafla hiyo.

Kwa mujibu wa Bw. Tenga, viwanda pia vinachangia asilimia 23 ya pato la kigeni linalotokana na mauzo ya bidhaa nje ya nchi na kwamba wao kama wazalishaji wanaunga mkono hatua zinazochukuliwa na serikali za kuondoa rushwa, kudhibiti matumizi na kuboresha nidhamu ya utumishi katika sekta ya umma.

Mwakilishi wa taasisi za kifedha zinazokopesha wazalishaji wa ndani na mmoja wa waandaaji wa tuzo hizo Bi. Jacqueline Woiso, yeye amezungumzia umuhimu na mchango wa taasisi hizo katika kutimiza ajenda ya serikali ya uchumi wa viwanda na kwamba zaidi ya asilimia 20 ya mikopo yote inayotolewa na benki anayoisimamia imekuwa ikienda kwenye sekta ya viwanda.