Alhamisi , 30th Oct , 2014

Tatizo la mimba za utotoni pamoja na kushuka kwa maadili nchini Tanzania. limedaiwa kuchangiwa na baadhi ya wazazi kutotenga muda wa kuzungumza na watoto wao juu ya changamoto zinazotokana na afya ya uzazi wakati wa makuzi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Afya ya Uzazi na Malezi nchini Tanzania - UMATI, Bi. Lulu Ng'wanakilala.

Mwenyekiti wa Chama cha Afya ya Uzazi na Malezi Bora nchini Tanzania UMATI Bi. Rose Wassira, amesema hayo leo wakati wa mkutano wa halmashauri Kuu ya chama hicho, mkutano unaoendelea jijini Dar es Salaam na kuwakutanisha viongozi na wanachama wa chama hicho kutoka mikoa yote nchini.

Bi. Wassira amesema utandawazi, harakati za kimaisha pamoja na aibu kumewafanya wazazi wengi washindwe kutenga muda wa kuzungumza na watoto wao kuhusu afya ya uzazi wakati wa makuzi, kiasi cha kusababisha maadili ya watoto hao kuharibika na hata wengine kujikuta wakipata mimba za utotoni na kujihusisha na tabia zisizoendana na maadili.

Kwa upande wake, mkurugenzi mtendaji wa UMATI Bi. Lulu Ngwanakilala amesema mkutano wa leo unakusudia kujadili masuala mbalimbali yanayohusu utendaji wa UMATI katika mwaka mmoja uliopita pamoja na kuangalia namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali.

Ametaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni kuzorota kwa huduma za afya ya uzazi hususani kwa vijana wadogo wa kike na wa kiume pamoja na matukio ya unyanyasaji na ukatili kwa watoto.

Amesema matukio ya ukatili kwa watoto yanaweza kupungua iwapo jamii itatekeleza kwa vitendo, harakati mbalimbali zinazofanywa na UMATI ikiwa ni pamoja na elimu kwa umma juu ya umuhimu wa wazazi kuwajibika katika ujenzi wa familia bora.

Aidha, hakusita kutaja mafanikio yaliyopatikana katika miaka michache iliyopita kuwa ni serikali kukubali wito wa UMATI wa kutaka kuongezwa kwa bajeti ya kufadhili upatikanaji wa huduma za uzazi wa mpango, hatua aliyosema imesaidia kujenga familia bora kupitia uboreshaji wa afya za akina mama.

Awali, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Bi. Pindi Chana amesema serikali haitakubali kuona vitendo vya ukatili kwa watoto vikiendelea katika jamii.

Amesema kupitia Katiba Inayopendekezwa, haki za mtoto zimetajwa wazi wazi na kwamba ukinzani wa kisheria kuhusu umri halisi wa mtoto nazo zimetajwa kikatiba.

Naibu waziri Chana amevishukuru vyombo vya habari kwa kile alichokitaja kuwa ni namna vilivyoelimisha umma kuhusu ukatili kwa watoto kiasi kwamba jamii imekuwa na uelewa kuhusu masuala hayo na sasa matukio ya unyanyasaji wa kijinsia na watoto yamekuwa yakiibuliwa kutoka kila kona ya nchi.