Jumamosi , 16th Apr , 2022

Jeshi la Polisi mkoani Njombe limeonya wananchi wenye tabia ya kuwaita wenzao wachawi na kusema kuwa mwananchi atakayegundulika kumuita jirani yake mchawi atakwenda jela miaka saba.

Sajenti wa Polisi Thobias Nyagawa kutoka idara ya dawati la jinsia na watoto amesema iwe mwisho kwa wananchi kusingiziana uchawi na endapo akibainika atakwenda jela moja kwa moja bila dhamana

Sajenti Nyagawa amesema hayo wakati Polisi na idara ya dawati la jinsia na watoto walipofika kijiji cha Itunduma kata ya Mtwango wilayani Njombe kutoa elimu juu ya unyanyasaji wa kijinsi, mauaji pamoja na udumavu mambo ambayo yamekuwa yakiwatesa wananchi mkoani humo.

“Kama kuna mtu anatangaza uchawi iwe mwisho, ukimwita mtu mchawi tukagundua, unakwenda jela miaka saba yaani hiyo unakwenda moja kwa moja hakuna dhamana” alisema Sajenti Thobias Nyagawa.

Kwa upande wake kamanda wa polisi mkoa wa Njombe Hamis Issah amewaonya vikali vijana wanao subiri kurithi mali za wazazi wao badala ya kufanya kazi ili waweze kujikwamua kiuchumi.