Alhamisi , 30th Apr , 2015

Vyama vinavyounda kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi UKAWA vya CUF, CHADEMA na NCCR Mageuzi, vimesema havina imani na Tume ya Taifa ya Uchaguzi NEC kwamba ina uwezo wa kusimamia mazoezi mbalimbali ikiwemo uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.

Viongozi kutoka vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi - UKAWA.

Wakizungumza katika mkutano wa pamoja waliouitisha jijini Dar es Salaam leo, wenyeviti wa taifa wa vyama hivyo wakiongozwa na Freeman Mbowe wa CHADEMA, viongozi hao wamesema NEC imejipotezea uhalali wa kuwa chombo kinachoaminika kuendesha chaguzi kutokana na kutoa kauli na ahadi ambazo haizitimizi.

Kwa mujibu wa Mbowe, kauli na ahadi zilizotolewa na tume hiyo hasa kuhusiana na zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura, zimekuwa za kutatanisha kwani kuna kipindi iliahidi kuwa zoezi hilo lingefanyika kama ratiba inavyoonesha lakini likaishia kuahirishwa kwa muda usiojulikana.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi James Mbatia ameitaka serikali kusogeza mbele zoezi la kura ya maoni hadi mwakani na kuachana na mpango wowote unaolenga zoezi hilo kufanyika mwaka huu.

Kwa mujibu wa Mbatia, katika kipindi hiki serikali inatakiwa ijikite zaidi katika maandalizi ya uchaguzi mkuu tena kwa kufanya mabadiliko ikiwa ni pamoja na kufanya mabadiliko ya tume ya uchaguzi iwe inayokubalika na kuaminika na wadau.