Meneja wa Tanesco Mkoa wa Ilala, Mhandisi Atanasius Nangali.
Meneja wa Tanesco mkoa wa Ilala mhandisi Atanasius Nangali, ameiambia East Africa Radio kuwa kazi ya ukarabati inaendelea vizuri ambapo mafundi wa shirika hilo wamekuwa wakifanya kazi usiku na mchana kuhakikisha umeme unarejea.
Ameyataja maeneo ambayo bado umeme haujarejea mpaka sasa kuwa ni Gongolamboto, Kivule na Kipunguni na kwamba muda wowote kuanzia sasa umeme katika maeneo hayo utarudi katika hali yake ya kawaida.
Kwa mujibu wa mhandisi Nangali, hitilafu hiyo ilisababisha maeneo mengi ya wilaya za Temeke, Ilala na Kisarawe kukosa nishati ya umeme, na kwamba juhudi zilifanyika za kurejesha umeme katika maeneo nyeti ikiwa ni pamoja na uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere ambako mafundi wa TANESCO mkoa wa Ilala waliandaa njia ya moja kwa moja ya umeme kutoka maeneo mengine ya jiji kuelekea uwanjani hapo.
Aidha, mhandisi Nangali amesema hitilafu hiyo ni ya kiufundi na kuongeza kuwa matukio ya aina hiyo yamekuwa nadra hivi sasa kwani shirika limeimarisha ukarabati wa miundombinu yake ikiwa ni pamoja na njia zilizochakaa pamoja na mifumo ya usambazaji.