Jumatano , 13th Mei , 2015

Wataalam wa mipango miji mkoani Arusha, jana walielezea wasiwasi wao juu ya ujenzi holela unaoendelea jijini humo, na kuitaka mamlaka husika kuchukua hatua za makusudi kutatua tatizo hilo.

Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Juma Iddi.

Wataalam hao walikuwa wakizungumza kwenye mkutano wa kwanza wa wadau kuhusiana na mradi ya kulipanga upya jiji la Arusha na viunga vyake.

Mkurugenzi wa jiji la Arusha, Juma Iddi, amesema Arusha ina heshima kubwa kitaifa na Kimataifa, hivyo ni vema ukapangwa katika mpango mzuri.

Amesema hatua za kwanza za kuutengeneza upya mji wa Arusha na viunga vyake, imetengewa shilingi bilioni 8 na serikali ya Tanzania, huku ikiwapa tenda ya kuboresha mji huo, Kampuni ya Surbana Interenational Consultants ya Singapore.

Juma amesema katika kuboresha jiji hilo ni vema kila mtaalamu na mwananchi kushirikiana na kuweka tofauti zao pembeni, bila kuangalia mipaka ya kazi zao, bali wanapaswa kutanguliza maslahi ya vizazi vijavyo.

Ameongeza kuwa kila hatua ya mradi huo itashirikisha wadau wa mipango miji na wananchi ili usikwame.

Naye mkuu wa mkoa wa Arusha, Daudi Ntibenda, katika hotuba yake iliyosomwa na mkuu wa Wilaya ya Arusha kwa niaba yake, Christopher Kangoye, amesema kazi ya kuanza mradi huo ilianza rasmi Desemba 15 mwaka 2014, baada ya kusainiwa kwa mkataba baina ya wizara ya Ardhi, Nyumba, Maendeleo na Makazi na kampuni hiyo ya Singapore.

Amesema kazi ya kulifanya jiji hilo liwe katika mpangilio mzuri, inatajia kukamilika ndani ya miezi 19 ijayo, hivyo vema kila mmoja akatekeleza majukumu yake ipasavyo.