Viongozi wakikagua ujenzi wa daraja la Pangani
Mradi huo unaotekelezwa na kampuni ya Ms Shandong Luqiua Group ya Kichina ulioanza Desemba mwaka jana na hadi kukamilika utachukua miezi 36 na utagharimu kiasi cha sh. 82,190,096,390.65.
Akisoma taarifa ya mradi huo mbele ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa Tanga Rajab Abrahaman Abdallah aliyeambatana na viongozi mbalimbali wa chama na serikali, Mhandisi wa TANROADS Safia Maliki amesema serikali itaugharamia mradi huo kwa asilimia 11.16 na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) itatoa fedha kwa asilimia 88.84.
Hata hivyo, alisema kuwa mradi unakumbana na changamoto mbalimbali ikiwemo kusafirisha mitambo ng'ambo ya pili pamoja na wafanyakazi lazima walipe kwenye kivuko, uhamishaji wa nguzo za umeme, makaburi na miundombinu ya maji.
Mara baada ya kukagua mradi huo wa daraja hilo katika ziara yake aliyoifanya wilayani Pangani Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Tanga Rajab Abrahamani Abdallah amepongeza uwepo wa mradi huo na kusema kuwa unakwenda kuwa mkombozi kwa wanapangani lakini pia watanzania wote kwa ujumla.
Mwenyekiti Rajab amesema wale wote wanaochukia sifa zinazotolewa kwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan wafike katika miradi inayotekelezwa na serikali wajionee mambo makubwa yanatekelezwa.
Alisema Chama cha Mapinduzi wakati ule kikinadi ilani yake na kuainisha miradi mbalimbali wapinga maendeleo ambao ni wapinzani walisema hayatawezekana jambo ambalo lilikuwa si kweli.