Ijumaa , 31st Aug , 2018

Balozi wa Uingereza nchini Tanzania ,Sarah Cooke, amesema kuwa lengo la ziara ya Waziri Mkuu wa nchi hiyo Mhe. Theresa May, katika baadhi ya nchi barani Afrika ni kuhakikisha wanasimamia na kuimarisha elimu kwa mtoto wa kike na kusisitiza usawa wa kijinsia.

Balozi wa Uingereza Tanzania, Sarah Cooke.

Akizungumza kwenye East Africa BreakFast ya East Africa Radio, Cooke, amesema kuwa Uingereza imeweka nguvu katika nchi za Afrika ili kuhakikisha suala la elimu linatekelezwa pasipo ubaguzi kwa watu wote hasa watoto wa kike na walemavu ambao wamekuwa wakifichwa kwenye baadhi ya jamii

Tunaimani kuwa misaada tunayotoa katika nchi za Afrika itaenda kuinua ubora wa elimu hususani kutoa fursa ya elimu kwa watoto wa kike na wenye ulemavu, huku tukiunga mkono pia juhudi za kupambana na rushwa, pamoja na kuboresha sekta za Afya”, amesema Cooke.

Agosti 10, 2018 Uingereza imetoa msaada wa shilingi Bilioni 307.5 kwa Tanzania kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za Rais Dkt. John Pombe Magufuli katika elimu, mapambano dhidi ya rushwa na uboreshaji huduma za afya, mbali na Bilioni sita zilizotolewa awali katika ujenzi wa shule ya sekondari Ihungo mkoani Kagera iliyojengwa upya baada ya kuharibika kufuatia tetemeko la ardhi lililotokea Septemba 2016.

Theresa May ametangaza mipango ya kuongeza vitega uchumi barani Afrika baada ya nchi yake kujiondoa Umoja wa Ulaya, ametoa ahadi hiyo nchini Afrika Kusini, ambayo ni kituo cha kwanza cha ziara yake ya barani Afrika na ameshatembelea nchi kadhaa ikiwemo Nigeria na Kenya.