Jumatatu , 20th Jul , 2015

Soko la hisa la Dar es salaam limekiri kuwepo kwa idadi ndogo ya wawekezaji katika soko hilo kutokana na dhana potofu kuwa wanaotakiwa kuwekeza ni watu wenye uelewa mpana wa fedha pekee.

Hayo yamesemwajijini Dar es salaam na Afisa Mtendaji Mkuu wa soko la hisa la Dar es Salaam (DSE) Bw. Moremi Marwa wakati wa hafla ya utoaji zawadi kwa washindi wa shindano juu ya uelewa kuhusu soko la hisa ambapo amesema dhana hiyo sio sahihi na imejengeka kutokana na kukosa elimu juu ya masuala ya elimu ya masoko ya mitaji.

Hata hivyo Marwa amesema kwa zaidi ya miaka 16 ya kuanzishwa kwa soko hilo ni kampuni 21 moja tu zilizoorodheshwa sokoni hapo ambapo kati ya hizo 14 pekee ndio kampuni za ndani.

Ameongeza kutokana na hali hiyo soko la hisa limeendelea kutoa uelimishaji ikiwemo kuanzisha kwa mashindano ya DSE Scola Investiment challenge ili kusaidia kuwafundisha vijana walio katika elimu ya vyuo vikuu ili waweze kuwahamasisha kuelewa dhana ya masoko ya mitaji na hisa.

Kwa upande wake mwanafunzi aliyeshika nafasi ya kwanza mashindano hayo Brigita Nchembi amesema zawadi walizopata zinawapa ari ya kuendeleza utoaji elimu kwa vijana wengine na kuweka jitihada za kuelewa juu ya matumizi ya mahesabu katika biashara, uwekaji rasilimali na uwekezaji.