Ijumaa , 19th Sep , 2014

Kamati ya Uandishi wa Rasimu iliyopendekezwa imesema kuwa hadi kufikiwa mwishoni mwa wiki ijayo watakua wamekamilisha kuandika rasimu iliyopendekezwa tayari kwa kupigiwa kura na wajumbe wa bunge maalumu la katiba.

Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi wa Rasimu ya Katiba Mpya, Andrew Chenge.

Mwenyekiti wa kamati hiyo Adrew Chenge amesema kuwa mpaka ikifika jumatatu ya tarehe 29 watakua wamekamilisha uandishi wa rasimu hiyo na kukabidhi kwa mwenyekiti wa bunge maalumu kwa ajili ya kuweza kuiwasilisha kwa wajumbe wa bunge hilo.

Mhe.Chenge amesema watanzania wategemee kupata katiba bora ambayo itakua na manufaa kwa taifa kwa kuwa imezingatia misingi muhimu ya kimaendeleo kwa mwananchi wa kawaida.

Wakati huo huo, wizara ya fedha na Uchumi nchini Tanzania imewataka waajiri katika taasisi za serikali kuhakikisha wanapeleka majina ya watumishi wao wanaostahili kulipwa mishahara kila tarehe kumi ya kila mwezi ili kuipusha serikali kulipa mishahara hewa.

Wito huo umetolewa jijini Dar es salaam na Naibu waziri wa Fedha na Uchumi Mwigulu Nchemba wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari juu ya kuwepo kwa baadhi ya taasisi za serikali ambazo zimekuwa zikipewa fedha za kulipa mishahara watumishi wake huku wengine wakiwa wameshafariki au kuacha kazi.

Aidha Naibu huyo waziri wa fedha na uchumi amewataka watumishi wa serikali kuhakikisha kila mmoja anakuwa na akaunti katika benki za hapa nchini kutokana na sasa serikali haitakuwa ikilipa mishahara kwa kutumia fedha taslim.