Jumatatu , 23rd Feb , 2015

ZOEZI la uandikishaji katika daftari la kudumu la kupiga kura lililoanza leo mkoani Njombe katika halmashauri ya mji Makambako limebainika kukumbwa na changamoto za vifaa kufanya taratibu na kusababisha mrundikano wa wananchi katika vituo.

ZOEZI la uandikishaji katika daftari la kudumu la kupiga kura lililoanza leo mkoani Njombe katika halmashauri ya mji Makambako limebainika kukumbwa na changamoto za vifaa kufanya taratibu na kusababisha mrundikano wa wananchi katika vituo vya kujiandikisha.

EATV Imeshuhudia wananchi wakiendelea na zoezi hilo kwa muda mrefu katika vituo vya kujiandikisha na kusema kuwa wanachelewa katika vituo hivyo kutokana na changamoto ya mashine hizo kutumia zaidi ya dakika 10 kwa kila mtu huku wengine mashine kushindwa kutambua vidole vyao.

Oraph Mhema amesema kuwa katika vituo walivyo kwenda kujiandikisha wameshidwa kuingiza maelezo yao ya kibaolojia na kuandikishwa kawaida kwa sababu ya mashine zinazo tumika kushindwa
kutambua vidole vyao kutokana na mikono yao kuwa na michilizi inayo tokana na shughuli za kila siku.

Amesema kuwa katika zoezi hilo kuna wasiwasi wa watu kushindwa kuandikishwa kutokana na muda unaotumika kwa mtu mmoja na muda uliopangwa kwa siku saba ambazo zitatumika katika halmashauri hiyo ya Makambako.

Mhema amesema kuwa mbali na changamoto ya mashine kufanyakazi taratibu pia katika zoezi hilo kugubikwa na watoa huduma hiyo kushindwa kuzitumia mashine kikamilifu kutokana na elimu ya kutumia mashine hizo kutowafikia mapema.

"Katika zoezi hilo wananchi wamehamasika kujiandikisha lakini wanakwamishwa na mashine hizo kufanya taratibu na baadhi yao kushindwa kuzitumia kikamilifu na nimeshuhudia mmoja akishindwa kubonyeza baadhi ya batani katika mashene," aliongeza Mhema.

Aliongeza : "Watu wengine wamechukuliwa taarifa nyingine kwa kuwa vidole vyao vimeshindwa kutambuliwa na mashine hizo kwa kuwa ina mikwaruzo mbalimbali inayotokana na ufanyaji wa kazi za kila siku," aliongeza.

Watu walio shindwa kutambuliwa na mashine wengi wao wamejaribu kurudia zaidi ya mara moja ambapo baadhi yao mashine zimekubali na wengine mashine zimeshindwa kabisa kutambuliwa,

Kwa upande wake mwananchi Sifaely Msigala amesema kuwa wananchi licha ya kujitokeza kwa wingi wameshindwa kuendelea na shughuli zao kutokana na kushinda muda mrefu katika uandikishwaji wa daftari hilo.

Amesema kuwa kama kasi ya mashine hizi itaendelea kuwa kama ilivyo, wananchi wengi huenda ukafika mwisho wakati hawajaandikishwa kutokana na mtu mmoja kutumia dakika nyingi katika kujiandikisha na kufanya zoezi hilo kuwaandikisha watu wachache katika daftari hilo.

Awali EATV ilifanikiwa kufika katika ofisi ya mkoa wa Njombe ili kujua ni idadi ya watu wangapi wangeweza kuandishishwa katika zoezi hili kulingana na takwimu za sensa ya watu mwaka 2012 ilishindwa kupata taarifa hizo kutokana na urasimu uliopo serikalini kwa kuambiwa aandike barua na maswali juu ya kile anachohitaji ilihali wahusika wanaweza kuzungumzia suala hilo wapo.

Kwa upande wa tume ya uchaguzi katika mji mdogo wa Makambako ambapo tume imekabidhi madaraka kwa mkurugenzi wa halmashauri husika, EATV imejaribu kumtafuta kwa simu kaimu mkurugenzi wa halmashauri hiyo Grace ambaye pia ni afisa utumishi wa halmashauri hiyo imemtafuta bila mafanikio ya kupokelewa kwa simu yake.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Njombe Dkt. Rehema Nchimbi amesema kuwa zoezi la uandikishaji wa Daftari la kudumu la kupiga kura kwa kutumia mfumo wa kieletronic BVR ambalo limeanza hii leo limepokelewa kwa muitikio mkubwa kwa wananchi kujitokeza kujiandikisha hasa vijana.

Akizungumza na East Africa Radio Dkt. Nchimbi amesema kuwa muitikio huo umetokana na uhamasishaji na uelimishaji juu ya umuhimu wa kujiandikisha katika daftari hilo ili kuweza kupata nafasi ya kuwachagua viongozi wanaowataka.

Aidha Dkt. Nchimbi ameitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi NEC kujiimarisha zaidi ili zoezi hilo lisikumbane na dosari kama zilizojitokeza wakati wa uandikishaji wa majaribio na kuongeza kuwa mpaka sasa hawajapata taarifa ya usumbufu wa vifaa ila ameahidi kufuatilia suala hilo kwa ukaribu zaidi