Jumatatu , 18th Apr , 2016

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, amewataka watanzania kujiepusha na upokeaji na utoaji wa rushwa kwa kuwa inawanyima haki baadhi ya wananchi na kudhoofisha ustawi wa nchi.

Makamu wa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Hassan Suluhu

Akiongea katika sherehe za uwashaji Mwenge wa Uhuru Mkoani Morogoro Mhe. Samia amewataka watumishi wa umma, watumishi wa sekta ya binafsi na wafanyabiashara kutekeleza majuku yao kwa kuzingatia katiba na taratibu zilizowekwa.

Bi. Samia amesema kuwa mkono wa serikali ya awamu ya tano hautamuacha mtu yeyote kwa cheo chake wala hadhi yake katika taifa na atawajibishwa endapo atabainika anajihusisha na vitendo vya rushwa.

Aidha Samia amewataka watanzania kumuunga mkono Rais wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli katika kukabiliana na vitendo vya rushwa na ufisadi ili kuokoa fedha zinazopotea kutokana na vitendo hivyo.

Makamu wa Rais amesema mpaka sasa jumla ya kesi 599 za rushwa zinaendelea mahakamani na jumla ya shilingi bilioni 9 na milioni 500 za kitanzania tayari zimeokolewa kutokana na kesi hizo.

Amesema kuwa serikali itaendelea kupambana na rushwa na ufisadi kwa nguvu zote lengo ikiwa ni kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato ya serikali na kuboresha uwajibikaji na maadili katika usimamizi wa rasilimali za umma na utoaji huduma kwa wananchi.

Ameongeza kuwa serikali itaendelea kufanya hivyo kwa mtindo wa utumbuaji majipu kwa kila atakayekwenda kinyume na taratibu za utumishi wa umma na kwamba utumbuaji huo hauna lengo la kumuonea mtu yoyote.

Sauti ya Makamu wa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Hassan Suluhu akizungumzia Rushwa.