Ijumaa , 6th Mar , 2020

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dkt Bashiru Ally, ameendelea kusisitiza kuwa hakuna mwanasiasa yeyote wa upinzani aliyezuiliwa kufanya mikutano jimboni kwake na kwamba ziara anazozifanya Polepole ni za kutangaza yale mazuri waliyoyafanya ndani ya chama.

Katibu Mkuu wa CCM Dkt Bashiru Ally

Dkt Bashiru ameyabainisha hayo leo Machi 6, 2020, wakati akizungumza kwenye mahojiano maalum yanayoruka mubashara kupitia vyombo mbalimbali na mitandaop yake ya kijamii vya Makampuni ya IPP, jijini Dar es Salaam.

"Mimi sidhani kama mikutano ya kisiasa imezuiliwa, Wabunge wanafanya mikutano kwenye majimbo yao na Polepole ni katibu wa Itikadi na Uenezi, anatangaza tunayoyafanya ili tusiondolewe madarakani, sasa mnataka akatangazie wapi chumbani? lazima ayatangaze hadharani" amesema Dkt Bashiru.

Aidha katika taarifa yake ya awali, Dkt Bashiru amevipongeza vyombo vya habari vya makampuni ya IPP kwa kuwa mstari wa mbele katika kusimamia haki na uongozi.