Ijumaa , 24th Jul , 2020

Waziri Mkuu Mstaafu Frederick Sumaye, ameeleza hisia zake kufuatia kifo cha Rais wa awamu ya Tatu Hayati Benjamin William Mkapa, ambaye amefariki Dunia usiku wa kuamkia leo katika moja ya Hospitali za Jijini Dar es Salaam, alikokuwa akipatiwa matibabu.

Kushoto ni Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Hayati Benjamin William Mkapa, na kulia ni Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye.

Sumaye amemtaja Mkapa kama kiongozi ambaye alichagiza mabadiliko makubwa katika mfumo wa utendaji na undeshaji wa Serikali na kuongeza kuwa Mzee Mkapa alikuwa kiongozi wakutegemewa, mwenye msimamo, asiyetetereshwa wala kuogopa katika uchapaji kazi.

''Binafsi nilifurahia sana kufanya kazi naye, kwa sababu alikuwa ni kiongozi mzuri anakuelekeza kama kuna mahali pana tatizo, lakini pia ni kiongzi ambaye kama unafanya kazi yako vizuri alikuwa hakuingilii kila mara, kulikuwa na uhuru wa kufanya kazi, kusimamia Serikali, kusimamia mambo ya utendaji wa Serikali bila ya uoga'' amesema Sumaye.

Hata hivyo amegusia changamoto mbalimbali ambazo ziliwakabili katika awamu ya tatu, ambapo miongoni mwa hizo ni pamoja na kifo cha Baba wa Taifa mwaka 1999, ukame Dar es Salaam uliopeleka Mto Rufiji kutopeleka hata tone la maji Baharini, pamoja na mvua ya Elnino.