Alhamisi , 5th Aug , 2021

Watu wawili wanashikiliwa na vyombo vya dola kwa tuhuma za kusafirisha shehena ya magunia 34 ya Tumbaku katika Mji mdogo wa Makongolosi wilayani Chunya, Mkoa wa Mbeya kwa kutumia njia za panya kuelekea nchi jirani ya Malawi.

Picha magunia yenye shehena za tumbaku yaliyokuwa yanasafirishwa kuelekea Malawi

Kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mayeka Simon amesema watuhumiwa hao wamekamatwa na shehena hiyo katika kizuizi cha barabara ya Mji Mdogo wa Makongolosi.

‘Tumekamata gari lililokuwa linasafirisha tumbaku ya ulanguzi, gari hili mmiliki wake ni Beni R Mwainga lenye namba T132 ADF na ni mwenyeji wa Mbeya, lilikuwa limebeba tumbaku ya Bw. John Mwambapa ikiwa na mitumba 34 yenye kilo 1603, tunaambiwa tumbaku hii inakwenda nje ya nchi na inasemekana inakwenda nchi ya Malawi,” amesema DC Simon.

Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Chama Kikuu cha Ushirika wa Wakulima wa Tumbaku Chunya, CHUTCU, Daniel Mpigasupi, ameeleza kuwa jambo kama hilo sio zuri kwani linamuumiza mkulima huku akiiomba serikali kuendelea kuchukua hatua ili kukomesha vitendo hivyo.

Naye Mkuu wa Idara ya Kilimo, wilayani humo, George Mwinuka akiwaonya wakulima pamoja na wafanyabiashara kuacha tabia ya kusafirisha zao hilo kwa njia ya panya.