Ijumaa , 8th Jul , 2016

Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) inatekeleza mkakati kabambe ambao utaongeza upatikanaji wa huduma na kushughulikia changamoto mbalimbali za wateja kwa wakati.

Akizungumza hayo katika Maonesho ya 40 ya Kibiashara ya Kimataifa ya Sabasaba, Bw. Aron Msonga Meneja Huduma kwa Wateja amesema kuwa kampuni inaendelea kuboresha miundombinu ya mawasiliano na yenye teknolojia ya kisasa ili kukidhi utoaji wa huduma bora na kwa wakati.

“Lengo letu kuhakikisha tunatoa huduma kwa wateja kwa uhakika na kwa wakati kwa kutumia teknolojia za kisasa zaidi, pamoja na kuendelea kutekeleza mkakati wa kushughulikia malalamiko ya wateja kwa wakati, ” amesema Bw. Msonga

Kuhusu kushughulikia malalamiko ya wateja, Bw. Msonga amewataka wateja wanaotumia huduma za TTCL endapo wakipata changamoto zozote kutoa taarifa kupitia namba 100, kutuma barua pepe au kutembelea kwenye kurasa za TTCL Za mitandao za kijamii, malalamiko hayo yatashughulikiwa kwa wakati.

“Kutokana na mkakati tulionao wa kuboresha biashara, kwa sasa hivi tunashughulikia malalamiko ya wateja wakati, kwa umakini na haraka zaidi ili wateja wetu waweze kupata huduma bora na kuongeza uzalishaji kwa maendeleo ya Taifa na kukuza pato la Taifa”amesema Bw. Aron Msonga.

Aidha, kwa sasa Kampuni inaendelea kushughulikia maeneo yote yanye changamoto ya mawasiliano, zoezi hilo ambalo limeanzia Dar es salaam na kisha kuelekea katika mikoa yote ya Tanzania.

Ushindi huu tuliopata kuwa Mshindi wa Kwanza katika sekta ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) inatupa nguvu ya kuongeza juhudi katika kuongeza ubora wa huduma zetu, kuboresha mtando wa mawasiliano na kuondoa kero kwa wateja wetu.

Awali, Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) ilizundua muenako mpya sambamba na huduma ya 4G ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Mkakati wa Mabadiliko ya Kibiashara unaendelea katika kampuni wenye lengo la kuboresha huduma za simu za mkononi, simu ya mezani na huduma za intaneti.