Jumatatu , 17th Feb , 2025

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa serikali kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu imetumia shilingi trilioni 8.2 kugharamia wanafunzi tangu ilipoanzishwa.

Waziri Mkuu Kssim Majaliwa

Amesema kuwa pia katika kipindi hicho wanafunzi takribani 830,000 wamenufaika na mfumo huo wa ugharimiaji wa elimu ya juu kupitia Bodi ya mikopo.

Amesema hayo leo Jumatatu (Februari 17, 2025) alipomwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye kilele cha maadhimisho ya miaka 20 ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, iliyofanyika kwenye Kituo cha Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam.

"Mafanikio tuliyonayo leo, ni matokeo ya utashi wa kisiasa, uongozi thabiti, maono na michango ya viongozi wetu. Viongozi wetu katika awamu zote walifanya kazi kubwa ya kuhakikisha Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu inafanya vizuri, viongozi wetu walioona mbali kuanzisha mfumo huu wa ugharimiaji wa elimu ya juu kupitia Bodi ya mikopo," amesema waziri Mkuu

Ameongeza kuwa katika kuhakikisha kuwa Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu haiwi mzigo kwa Wanafunzi, Serikali iliamua kufuta tozo za kulinda thamani ya fedha ili kuondoa changamoto katika urejeshaji wa mikopo. “Kwa sasa mnufaika anarejesha kiasi kile kile ambacho amekopeshwa kwani tozo hizo zilikuwa zinasababisha ongezeko la madeni ya mikopo hiyo.”