Jumatatu , 30th Mei , 2016

Serikali ya Tanzania imepokea msaada wa Shilingi Bilioni 7.4 kwa ajili ya kufanya utafiti wa viashiria na matokeo ya hali ya Virusi vya Ukimwi kuanzia watoto wa changa hadi wazee.

Akiongea wakati uzinduzi wa utafiti huo Mkurugenzi Mkuu wa ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Dk. Albina Chuwa amesema utafiti huo utafanyika kwa muda wa mwaka mmoja ili kutoa fursa kwa serikali kujua kiwango cha ugonjwa wa Ukimwi nchini na jinsi ya kujiwekea kiwango cha maendeleo.

Dk. Albina amesema, lengo la kuhusisha umri wa watoto wa changa na kuendelea ni kuiwezesha serikali kujua, maambukizi mapya ya virusi vya ukimwi, tabia za watu na unyanya paa, idadi ya wanaotumia dawa za kupunguza makali ya Virusi vya Ukimwi na kiwango cha kinga kwa waadhirika wa virusi vya Ukimwi.

Naye Mkurugenzi wa Tume ya kudhibiti Ukimwi nchini (TACAIDS) Bi. Fatma Mrisho amesema, wanatarajia kufikia malengo ya kuwa na sifuri tatu ifikapo mwaka 2020 ya kuondokana na vifo vitokanavyo na virusi vya Ukimwi, unyanyapaa kwa waathirika wa Ukimwi na maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi.

Wananchi kwa ujumla wameombwa kutoa ushirikiano kwa wataalam na watafiti ambao watatembelea maeneo mbalimbali nchini kwa upande wa Tanzania bara na Tanzania visiwani ili kuiwezesha serikali kuwa na takwimu mpya juu ya ugonjwa huo.