Taarifa hiyo imethibitishwa na mgombea Ubunge wa Jimbo la Kinondoni ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Salum Mwalimu alipowasili katika kipindi cha 'East Africa Breakfast' kinachorushwa kutoka East Africa Radio.
"Ni kweli Tambwe Hizza amefariki nami nimetumiwa ujumbe mfupi mara nilipofika hapa East Afrika Radio kama kiongozi wa chama, hivyo naomba tupewe muda kidogo ili tuweze kufahamu zaidi chanzo cha kifo chake maana imekuwa ghafla sana kutokana mpaka jana usiku saa 5 nilikuwa nae", amesema Mwalimu.
Kwa upande mwingine, Salum Mwalimu amesema mpaka jana marehemu Tambwe Hizza alikuwa nae katika kuomba ridhaa kwa wananchi wa jimbo la Kinondoni ili aweze kuwa Mbunge wa Jimbo hilo katika siku za usoni.
Marehemu Tambwe Hizza amefariki akiwa ni mmoja wa waratibu wa kampeni za chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA) katika jimbo la Kinondoni
Hizza anafahamika sana kwa siasa zake akiwa CUF, Baadae alihamia CCM na kuwa Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Propaganda wa CCM na 2015 aliamua kuondoka CCM na kuhamia CHADEMA. Mwaka 2014 alisema angegombania Urais kupitia cha mapinduzi kwani uwezo, akili, elimu na afya ya kumuwezesha kuwa Rais wa tano wa Tanzania.

