Alhamisi , 4th Jun , 2015

Uzalishaji na tija ndogo katika zao la pamba nchini Tanzania umetajwa kuwa kikwazo kikubwa kinachosababisha wakulima kupata faida ndogo na hivyo kutokidhi gharama za uzalishaji.

Zao la Pamba

Kauli hiyo imetolewa leo bungeni na naibu waziri wa Wizara ya kilimo, chakula Godfrey Zambi ambapo mpaka sasa wastani wa uzalishaji wa zao la pamba ni kilo 250 mpaka 300 kwa hekari ikilinganishwa na uzalishaji wa tija wa kilo 800 mpaka 1000 hivyo kutowezesha wakulima kupata faida hata wakati bei ya pamba inapoongezeka.

Amesema mpaka sasa serikali imeweka mkakati kupitia bodi ya pamba wa kuanzisha shamba darasa katika kila halmashauri ili kushughjulikia changamoto ya tija katika uzalishaji wa zao la pamba ili kukidhi viwango vya ushindani katika soko la dunia.

Hata hivyo Zambi amevitaka viwanda vinavyozalisha nguo nchini kuweka mkakati na jitihada za kutumia pamba inayozalishwa nchini kwa kutengeneza nyuzi na nguo mbalimbali ili kusaidia katika kukuza soko la ndani na kuwasaidia wakulima kulithamini zao la pamba.