Ijumaa , 28th Jul , 2023

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile amesema kuwa uhuru wa vyombo vya habari umeongezeka nchini hivyo ni jukumu la waandishi wa habari kuwajibika na kuzingatia sheria zilizopo.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile

Balile ametoa kauli hiyo  jijini Dar es Salaam wakati wa Muungano wa Haki ya Kupata Habari (CoRI) wakijadiliana juu ya marekebisho ya Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 iliyofanyiwa marekebisho mwezi uliopita.

Amesema wanahabari hawapaswi kuchafua taaluma yao kwa kutofanya kazi kwa weledi au kutumia vibaya uhuru ulioongezeka hivi sasa baada ya miaka sita migumu na sheria ngumu.

"Ni ukweli usiopingika kuwa uhuru umeanza kuimarika, watu wanazungumza kwa namna wanavyotaka na wengine wamefikia hatua hata kutoa kauli zisizofaa kwa viongozi na hawakamatwi na polisi kama ilivyokuwa miaka sita iliyopita, nawaomba waandishi wenzangu tutumie fursa hii vizuri kwani tukifanya tofauti Serikali inaweza kufanya marekebisho na kurejea kule tusikokutaka," amesema Balile

Serikali imekiondoa kifungu cha 5(1) kilichokuwa kikimpa mamlaka Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), kugawa matangazo kwenye vyombo vya habari ambapo mwanya huo uliviumiza vyombo vingine vya habari lakini sasa kimeondolewa na mambo yameanza kuwa vizuri.

Naye Deus Kibamba amewataka waandishi wa habari kuwa wabunifu katika utendaji kazi, kutetea haki zao, kulinda na kukuza tasnia yao ili wapige hatua zaidi.

Deus Kibamba alisema mabadiliko ya sheria yaliyofanywa na Serikali hayatakuwa na maana kama waandishi wa habari hawatakuwa wabunifu na kujiandaa kwa mabadiliko yatakayotokea.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Tumaini (Tudarco), Dk Darius Mukiza amesema vyombo vya habari hivi sasa vinapaswa kutafuta njia ya kuboresha mapato yake na kukuza ajira.