Mamlaka ya Mawasiliano TCRA imevifungia vituo 21 vya Radio na 6 vya TV kwa kushindwa kulipa kodi ya lesseni kwa wakati.
Akitangaza uamuzi huo, mkurugenzi wa habari na mawasiliano wa TCRA Innocent Mungy, amesema kuwa mitambo ya vituo hivyo itazimwa ifikapo kesho saa 6 usiku, na itawashwa baada ya vituo hivyo kulipa madeni yanayowakabili.
Mungy amesema mamlaka hiyo haiwezi kusema ni kiasi gani cha pesa ambacho vituo hivyo vinadaiwa kwa madai kuwa kanuni na taratibu haziwaruhusu kutaja kiasi hicho kwa kuwa ni siri kati ya TCRA mteja.
Ameongeza kuwa makampuni hayo yalipewa taarifa tangu mwezi Julai mwaka jana juu ya kulipa madeni hayo lakini ni kampuni mbili pekee (ambazo hakuzitaja majina) zilizolipa, na nyingine hazijalipa hadi sasa, na hivyo kuilazimu mamlaka hiyo kuchukua hatua ya kuzifungia kwa miaezi mitatu hadi zitakapolipa madeni.
Mungy amesema kuwa hapo awali vilikuwa vyombo 40 amabavyo havikutekeleza agizo lakini vyombo 11 vikalipa huku vyombo 27 vikionekana kukaidi agizo la mamlaka hiyo hali iliyopelekea kufungiwa kwake.
Amesema kuwa kwa kampuni ambazo zitashindwa kulipa ndani ya miaezi mitatu zitanyanganywa leseni moja kwa moja.
Aidha Mungy amesema kuwa TCRA imewataka wadau wote wa mawasiliano nchini kutii sheria bila shuruti na kufuata taratibu, huku akisisitiza kuwa zoezi hilo la kuwasaka wanaokwepa kodi ni endelevu.