Jumamosi , 15th Mar , 2014

Mamlaka ya mawasiliano nchini Tanzania TCRA imetahadharisha wananchi juu ya kuwepo kwa tabia ya baadhi ya watu kusajili kadi zao za simu na kwa kutumia majina bandia.

Profesa John Nkoma,Mkurugenzi Mkuu wa TCRA

Mkurugenzi mkuu wa TCRA Prof: John Nkoma ametoa tahadhari hiyo jana jijini Dar es salaam wakati alipokutana na wahariri na waandishi wa habari kuzungumzia siku ya mtumiaji wa huduma za mawasiliano duniani iliyoadhimisha rasmi jana.

Prof: Nkoma amesema kitendo hicho kimesababisha watu wengi kukosa haki zao pale wanapotumiwa fedha kwa njia ya simu kutokana na kusahau jina alilosajili huku wengine wakitumia usajili huo wa majina bandia kwa kuwatukana viongozi wakuu wa kitaifa na wananchi wa kawaida

Aidha katika hatua nyingine mamlaka hiyo ya mawasiliano imesema kuna haja kwa Tanzania kuwa na sheria inayotambua haki za mtumiaji wa simu ambayo itasaidia kumlinda mtumiaji na kupata haki zake kama vile za huduma bora ya mawasiliano, usalama pamoja na kujua tozo za simu kabla ya kutumika.