Jumatatu , 4th Dec , 2017

Mkurugenzi wa wakala wa Majengo nchini Mhandisi Elius A. Mwakalinga ameondoa mzozo uliopo kwa baadhi ya watu kuhusu gharama kamili za ujenzi wa mabweni ya chuo kikuu Dar es salaam, na kusema kwamba gharama iliyotajwa siku ya uzinduzi ndio sahihi.

Akizungumza na mwandishi wa East Africa Television, Mhandisi Mwakalinga amesema wao kama waliofanya ujenzi wa majengo hayo pesa walizopewa kuweza kukamilisha ujenzi huo ni bilioni 10, na sio ambazo watu mbali mbali wamekuwa wakizitaja.

Akiendelea kuzungumzia hilo Mhandisi Mwakalinga amesema watu ambao wanaibua masuala kama hayo walikuwa wanataka mianya ya kupiga hela lakini wameikosa, na kwamba watu walitakiwa kuwapongeza kwa kufanikisha hilo na sio kusambaza habari za uongo.

Sisi tumepewa bilioni 10 ambao ndio tumefanya shughuli zote za ujenzi, kwa nini watu wanaamini maneno ya watu ambayo hata hawakuwa part of this!? Watu wanaosema haya mambo walikuwa wanaibia serikali, walikuwa wakitangaziwa tenda basi wakishaanza kulipwa kwanza wanaenda Dubai kusherehekea, sasa wanakosa hizo fursa lazima wataongea hivyo, wamekosa mianya ya kupiga hela, kwanza walitakiwa watupongeze, mwanzo walisema hawataweza sasa tumeweza hawataki kutupongeza”, amesema Mwakalinga.

Hivi karibuni kumeibuka mjadala mkubwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu gharama halisi za ujenzi wa mabweni hayo, ambapo taarifa rasmi iliyotolewa na serikali siku ya uzinduzi ni sh. bilioni 10, huku kukiwa na tetesi kwamba zimetumika bilioni 59.