Jumatatu , 23rd Mar , 2015

Tanzania imepokea silaha za kivita bunduki aina ya AK 47 pamoja na magari matano aina ya land cruiser pickup, vifaa vitakazosambazwa katika mapori ya akiba pamoja na vikosi vya kupambana na ujangili ili kukabiliana na matukio ya mauaji ya ujangili.

Waziri wa Maliasili na utalii Lazaro Nyalandu.

Waziri wa Maliasili na utalii Lazaro Nyalandu akikabidhi vifaa hivyo katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro KIA,amesema wajibu uliopo ni kuhakikisha wananchi pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama wanashirikiana ili Tanzania iweze kudhibitii utoroshwaji wa nyara za Serikali na kutunza rasilimali kwaajili ya vizazi vyote vijavyo.

Nyalandu pia ametoa mwito wa kuwepo kwa uwajibikaji wa pamoja ili kuongeza ufanisi wa kuwatumikia wananchi kwa kufuata ilani ya chama cha mapinduzi kinachoongoza Serikali katika kuhakikisha uhifadhi unakuwa endelefu na pia wananchi kuweza kunufaika moja kwa moja na rasilimali za taifa.

Baadhi ya Askari akiwemo Michael Msokwa ambaye ni Naibu Mkuu wa kikosi cha kupambana na ujangili Kanda ya Kaskazini wamesema vifaa hivyo ni vyenye ufanisi Mkubwa na kwamba vitawawezesha kupambana na matukio ya mauaji ya wanyamapori katika maeneo mbalimbali nchini.

Wakati vifaa hivyo vikikabidhiwa ripoti ya robo mwaka ya kikosi cha kupambana na ujangili kanda ya kaskazini inaonyesha kwamba matukio ya mauaji ya wanyamapori bado yapo huku majangili wapatao 203 wakiwa wamekamatwa na kufikishwa mahakama.