Jumatano , 30th Mar , 2016

Serikali ya Tanzania na Kuwait zimetiliana saini mkataba wa ushirikiano katika sekta ya usafiri wa Anga ambao utasaidia kupanua fursa za biashara miongozni mwa nchi hizo mbili.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa.

Akizungumza katika utilianaji saini wa Mkataba huo Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa amesema kuwa Mkataba huo ni fursa nzuri ya kibiashara kati ya nchi hizo mbili ambapo Kuwait Airways itaanza safari za moja kwa moja kutoka nchini humo kuja Tanzania.

Aidha Waziri Makame ameongeza kuwa licha ya ushirikiano wa kibiashara,sekta hiyo ya usafiri wa anga itasaidia kukuza utalii wa Tanzania na kuliongeza taifa pato kwa kiasi kikubwa.

Amesema kuwa Mkataba huo pia unajumuisha mpango wa kubadilishanas uzoefu kati ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania TCAA na Kuwait katika mafunzo ya muda mfupi kwa watumishi wake.

Waziri huyo amesema kuwa katika kipindi cha miezi miwili ijayo ATC,itakua na ndege mbili zinazotoa huduma za ndani ya nchi baadae nyingine zitafanya safari katika ukanda wa Afrika Mashariki baadae nje ya nchi ikiwemo Dubai, Kuwait na Bombay.