Jumatatu , 29th Dec , 2014

Tanzania ndiyo nchi pekee ambayo bado inayowauzia wananchi wake mafuta kwa bei ya juu licha ya bei ya mafuta katika soko la dunia kushuka kwa zaidi ya asilimia 50.

Mbunge wa Mbeya mjini, Joseph Mbilinyi maarufu kama Sugu.

Mbunge wa Mbeya mjini, Joseph Mbilinyi ameyasema hayo wakati akiongea na Wananchi wa Halmashauri ya mamlaka ya mji mdogo wa Kyela na kusema kuwa kumekuwepo na bei kubwa ya mafuta nchini ikilinganishwa na nchi nyingine.

Mh. Mbilinyi, amedai kuwa bei hiyo ya mafuta ni kubwa ikilinganishwa na nchi nyingine duniani ambazo gharama za mafuta zimeshuka zaidi ya nusu kutoka na kupatikana kwa wingi kwa bidhaa hiyo kwa sasa duniani.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Mbeya, Joseph Mwachembe maarufu kwa jina la China amesema kuwa katika maeneo ambayo CHADEMA imeshinda kuongoza serikali za mitaa na vijiji, viongozi wake watafanya kazi kwa kuzingatia matakwa ya wananchi na sio maelekezo kutoka serikali kuu.

Nao viongozi wa UKAWA mkoani Mbeya wamesema kuwa muungano wa vyama vinavyounda umoja huo umeonesha mafanikio makubwa kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa na moto huo huo utaendelea mpaka kwenye uchaguzi mkuu ujao.