Alhamisi , 29th Sep , 2022

Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika zitakazonufaika na fedha za mfuko wa kukuza uwekezaji barani Afrika kutoka serikali ya Japan zitakazotolewa kuanzia Machi, 2023 ambazo ni takribani dola Milioni 100.

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa na Viongozi wengine nchini Japan

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa timu ya Afrika ya KEIZAI DOYUKAI (Japan Association of Corporate Executives), Bw. Mutsuo Iwai wakati akizungumza na Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa ofisini kwao Marunouchi, Chiyoda-ku, jijini Tokyo, Japan.

Aidha amesema fedha hizo za uwekezaji kwenye mitaji (start-ups) zimelenga kukuza biashara ambazo zitatatua changamoto za kijamii zikiwemo sekta za afya, kilimo, nishati na kuimarisha uhifadhi wa mazingira.

Utolewaji wa fedha hizo ni utekelezaji wa ahadi ya Waziri Mkuu wa Japan, Fumio Kishida aliyoitoa Agosti 27, 2022 wakati akitoa hotuba kwenye Mkutano wa Nane wa Kimataifa wa Wakuu wa Nchi na Serikali unaohusu Maendeleo ya Japan na Afrika (TICAD 8) uliofanyika jijini Tunis, nchini Tunisia.

Waziri Mkuu pia alikutana na wawakilishi wa Shirikisho la Wafanyabiashara wa Japan (KEIDANREN) ofisini kwao Otemachi, Chiyoda-ku, jijini Tokyo, ambako Mwenyekiti wa Kamati ya nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara, Bw. Hajime Kawamura alimweleza jinsi shirikisho lao linavyojihusisha na miradi ya maji, barabara, nishati, mawasiliano utengezaji wa kemikali na ununuzi wa mazao.