Ameyasema hayo leo (Alhamisi, Februari 6, 2025) wakati akijibu swali la Mbunge wa Mbozi, George Mwanisongole katika kipindi cha maswali kwa Waziri Mkuu Bungeni jijini Dodoma.”Tanzania itatumia vyanzo vya fedha na mapato vilivyowasilishwa Bungeni ili vipangiwe kazi ili kujazia maeneo yaliyopungua.”
Mbunge huyo alitaka kujua Serikali inajipangaje na mabadiliko ya sera za nje ya nchi ya Marekani ambayo yanakwenda kuathiri utekelezaji wa sera za elimu, afya na uchumi hususan miradi ya maendeleo inayofadhiriliwa USAID.
”Uwezo tunao, tunazo maliasili, tunazo rasilimali, kazi ambayo tunayo ni Watanzania kushirikiana kuhakikisha tunatumia maliasili na rasilimali tulizonazo kujenga uchumi wa ndani kuwezesha mipango na bajeti iweze kutekeleza haya.”
Amesema Tanzania inaheshimu sera za mambo ya nje na inatekeleza mikataba kwa mujibu wa sera hizo kama ilivyokubaliana na nchi husika katika maeneo mbalimbali. ”Tumeanza kuona nchi zenye uwezo mkubwa ikiwemo Marekani ikibadilisha sera zao na mabadiliko yake yanathiri baadhi ya nchi, kwetu sisi ni muhimu kuzingatia sera za nje na kuzitekeleza kama tulivyokubaliana.”
Pia, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuifanya Tanzania kuwa na mahusiano na nchi nyingi duniani na Marekani ni moja kati ya nchi hizo.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Kilimo iendelee kutoa elimu kuhusu uendeshwaji wa mfumo wa stakabadhi ghalani katika maeneo yote ambayo wanataka mazao yauzwe kwa kupitia mfumo huo ili kuondoa migogoro kwa wakulima.
Ametoa agizo hilo wakati akijibu swali la Mbunge wa Sumve, Kasalali Mageni aliyetaka kufahamu kauli ya Serikali kuhusu taharuki iliyojitokeza baada ya mazao ya choroko kuwekwa katika mfumo wa stakabadhi gharani kwa kuwa zao hilo ni chanzo cha chakula na akiba.
Waziri Mkuu amesema kwenye sekta ya kilimo yapo mazao ya biashara na chakula, pia yapo mazao ya chakula yanatumika kwa biashara, Serikali imeendelea kuimarisha masoko ya mazao kwa kutumia mifumo mbalimbali kufanya biashara za mazao hayo zikiwemo choroko.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema anatambua yapo baadhi ya maeneo ambayo yana migogoro inayowafanya wakulima washindwe kuamini mfumo huo, hivyo ameiagiza Wizara ya Kilimo kuendelea kutoa elimu kwa wakulima ili kuondoa taharuki.
Amesema choroko ni miongoni mwa mazao ambayo Serikali imekuwa ikiratibu biashara yake pale ambapo mwananchi ameamua kutumia kama zao la kibiashara kupitia mifumo ya mauzo iliyopo kama kilimo cha mkataba au kuuza mkulima kuuza ndani na nje ya nchi.
”Upo mfumo ambao sasa tunautumia kwa mazao mengi wa minada na minada hii ili iende vizuri tuliona tutumie mfumo wa stakabadhi ghalani mfumo ambao unawezesha wakulima kupata faida kubwa kutokana na ushindani wa wanunuzi unaofanyika kwa njia ya mnada.”
Katika hatua nyingine, Mhehimiwa Majaliwa amesema kuwa Serikali itaendelea kuhamasisha uwekezaji kwenye viwanda ili kuweza kuyanusuru mazao ambayo yanaharibika kwa haraka ikiwemo parachichi.