Jumanne , 27th Mei , 2014

Serikali ya Tanzania imesema mpaka kufikia Machi 2014 imeshapeleka askari 2,259 katika nchi mbalimbali za Afrika na Duniani katika kuusaidia Umoja wa Mataifa katika utatuzi wa migogoro na ulinzi wa amani.

Waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa wa Tanzania, Bernard Camillius Membe.

Hayo yameelezwa leo Bungeni Mjini Dodoma na Waziri wa Mambo ya nje na Ushirikiano wa Kimataifa,Mhe Bernard Membe wakati akitoa hotuba ya makadirio ya Bajeti ya Wizara yake, kwa mwaka wa fedha 2014/15.

Naye Msemaji wa Kambi rasmi ya upinzani bungeni kwa Wizara ya Mambo ya nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe Ezekiah Wenje wakati akitoa hotuba ya kambi hiyo, ameitaka serikali kutoa kauli juu ya tuhuma alizozieleza kuwa Mhe. Berdard Membe amenukuliwa akisema anaamini kuwa kundi la M23 ni Wanyarwanda na si raia wa DRC.

Mbunge wa Nkasi kupitia CCM, Ally Kessy akichangia hotuba hiyo amesema Serikali iendelee kutoa msaada kwa nchi zenye migogoro kutokana na wananchi wa Tanzania wanaoishi mipakani kupata usumbufu mkubwa katika kuwasaidia wakimbizi wanasababishwa na vita nchini DRC .