Alhamisi , 4th Sep , 2014

Tanzania imefanikiwa kupunguza maambukizi ya ugonjwa wa malaria kwa zaidi ya asilimia hamsini ingawa bado ugonjwa huo ni moja ya magonjwa hatari na yanayouwa watu wengi zaidi nchini.

Mkurugenzi wa taasisi ya afya ya Ifakara, Dkt Salim Abdullah.

Kaimu Mkurugenzi Idara ya Kinga kutoka wizara ya afya na ustawi wa jamii Dkt. Neema Rusibamayila, amesema hayo leo wakati wa mkutano wa kimataifa kuhusu malaria unaondelea jijini Dar es Salaam ambapo ametaja sababu za kupungua kwa malaria kuwa ni kutokana na matumizi ya vyandarua vyenye dawa pamoja na kampeni mbalimbali zinazoendeshwa na wizara ya afya katika kukabiliana na ugonjwa huo.

Kwa mujibu wa Dk. Rusibamayila serikali hivi sasa imeweka mkazo kuhakikisha dawa za malaria zinaolewa kwa walliodhibitika kuwa na ugonjwa wa malaria ili kupunguza usugu wa ugonjwa unaotokana na unywaji holela wa dawa za malaria.

Kwa upande wake, mkurugenzi mkuu wa taasisi ya afya ya Ifakara Dkt Salim Abdulla, amesema taasisi yake inaendelea na tafiti kadhaa zinazolenga kupunguza maambukizi ya ugonjwa wa malaria nchini.

Moja ya tafiti hizo kwa mujibu wa Dkt Abdulla ni ile inayolenga kuja na mbinu pamoja na njia rahisi za kupunguza kiwango cha mbu wanaoingia katika nyumba na makazi ya watu, kama njia pekee ya kupambana na ugonjwa wa malaria baada ya mbinu zilizopo sasa kujikita zaidi katika kuzuia mbu kung'ata watu wakati wakiwa wamelala.

Dkt Abdulla ametaja tafiti nyingine kuwa ni zile zinazoangalia tiba za ugonjwa wa malaria, ili kuweza kuja na tiba sahihi katika kupunguza ukubwa wa ugonjwa huo, hususani tabia ya mara kwa mara ya vijidudu vya magonjwa kujenga usugu dhidi ya dawa.