Jumatatu , 20th Apr , 2015

Shirika la umeme Tanzania (TANESCO) mkoa wa Iringa na Njombe kwa kushirikiana na Mpango wa Umeme Vijijini REA linatarajia kuboresha huduma zake ili kuongeza idadi ya wateja wake wa mjini na vijijini.

Wahandisi wa Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) wakiwa katika mazoezi mbalimbali ya kubaini nguzo bora.

Meneja wa shirika la umeme mkoa wa Iringa Bi.Sarah Assey amesema kwa upande wa shirika hilo kwa mkoa wa Iringa kwa sasa lina wateja 63,300 na mpango mkakati ni kuwafikia wateja 30,000 hali itakayopelekea kuwa na jumla ya wateja 930,000.

Bi. Assey amesema kutokana na gharama za uunganishwaji wa huduma za umeme serikali imeamua kuwafikia wakazi wa vijijini kwa punguzo la VATA kwa huduma hiyo ili kurahisisha shughuli za uzalishaji mali na kuongeza uchumi wao.

Aidha ameongeza kuwa shirika linaendelea na uunganishaji wa huduma za umeme kwa wateja wapya wa mjini pia serikali inaendelea kuboresha maisha ya wananchi kwa kupunguza gharama za utumiaji wa umeme kwa wateja wenye matumizi chini ya unit 75 kwa mwezi.

Hata hivyo, Meneja wa TANESCO mkoa wa Iringa ametoa wito kwa wateja kushirikiana na shirika hilo kupunguza upotevu wa nishati hiyo inayofanywa na baadhi ya wafanyakazi wasio waaminifu na vishoka wa mtaani ambao hutumia jina la umeme.