
Mafundi wa shirika la umeme nchini Tanesco wakirekebisha moja ya miundombinu iliyopata hitilafu
Taarifa ya kaimu meneja wa Tanesco Ilala Bw. Ahmed Mningwa, imetaja chanzo cha kukosekana kwa huduma hiyo kuwa ni kutokana na hitilafu kubwa kwenye moja ya transfoma za kusambaza umeme katika kituo kikubwa cha Ilala.
Maeneo yaliyoathirika ni Buguruni, Vingunguti, Kiwalani, Sukita, viwanda vyote vilivyo kokandokando ya barabara ya Mwalimu Nyerere hadi Kipawa, kigamboni, Mkuranga, Mbagala, Mtoni Kijichi, ofisi za Manispaa ya Temeke, Uwanja wa Taifa, JKT Mgulani, baadhi ya maeneo ya Keko na Chang’ombe, na Viwanda vyote vilivyoko kandokando ya barabara ya Bandari, Kurasini na baadhi ya maeneo ya Mtoni Mtongani.
Mningwa amefafanua kuwa kutokana na kutambua kadhia wanayopata wananchi wa maeneo hayo, mafundi wa shirika la umeme nchini wanaendelea na shughuli ya ukarabati wa sehemu iliyopata hitilafu ili kuhakikisha kuwa huduma za umeme katika maeneo yaliyoathirika zinarejea kama kawaida.