Jumatano , 11th Jun , 2014

Ofisi ya taifa ya takwimu imefafanua sababu zilizochangia kuongezeka kwa umri wa kuishi nchini, kutoka kiwango cha awali cha miaka hamsini hadi umri wa miaka sitini na mmoja, kama ilivyobainishwa kwenye chapisho kuu la sensa ya watu na makazi.

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiteta jambo na mkurugenzi mkuu wa ofisi ya taifa ya takwimu NBS Dkt Albina Chuwa (kulia) wakati wa uzinduzi wa chapisho kuu la sensa ya watu na makazi jijini Dar es Salaam jana.

Mratibu wa sensa kutoka ofisi ya taifa ya takwimu Bw. Irenius Ruyobya, amezitaja sababu hizo kuwa ni hali bora ya uchumi inayoambatana na kuongezeka kwa pato la mtu mmoja mmoja pamoja na huduma bora za afya na makazi huku akizitaja huduma duni ilizokuwepo hapo awali kuwa zilichangia idadi kubwa ya watu kufa wangali wakiwa na umri mdogo.

Aidha, Bw. Ruyobya amesema licha ya kuongeazeka kwa umri wa kuishi, matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 inaonyesha kuwa watu milioni 44 ambayo ni sawa na asilimia tisini ya watu wote nchini ni vijana waliozaliwa baada ya mwaka 1964, kizazi kinachotajwa kuwa ni cha muungano kutokana na kuzaliwa baada ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar.