Jumatano , 2nd Oct , 2019

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Ilala, imesema kuwa iko mbioni kukamilisha ufuatiliaji wa uchunguzi wa miradi miwili, ikiwemo ujenzi wa machinjio ya kisasa ya Vingunguti unaogharimu kiasi cha Shilingi bilioni 12,pamoja na soko la Kisutu.

RC Makonda akiwa kwenye mradi

Taarifa hiyo imetolewa leo Oktoba 2, 2019 na Kamanda wa TAKUKURU Ilala, Christopher Myava, ambapo amesema lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha inaziba na kuzuia mianya yote ya rushwa katika miradi hiyo.

''Tutakamilisha ufuatiliaji wa miradi ya ujenzi wa machinjio ya kisasa ya Vingunguti ambao una thamani ya Shilingi bilioni 12, kama mnavyofahamu mradi ule unafuatiliwa  kwa karibu sana na sisi kama TAKUKURU tunataka kuhakikisha hakuna uvujaji wa pesa za umma, pia tutaendelea kufanya ukaguzi wa ujenzi wa  soko la Kisutu" amesema Kamanda Myava.

Aidha katika kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, TAKUKURU mkoani humo, imejidhatiti kufuatilia hatua kwa hatua ili kuhakikisha uchaguzi unafanyika salama na kuwataka wapiga kura na wagombea, kuhakikisha wanajiepusha na vitendo vya rushwa.

Hatua hii imekuja baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli, kuonesha kutoridhisha na kasi ya utekelezaji wa mradi wa machinjio hayo na ndipo Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda, alipoanzisha kampeni ya tukutane 'Site' kwa kufanyakazi usiku na mchana ili miradi hiyo ikamilike.