Jumatatu , 20th Mar , 2023

Serikali kupitia Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imesema imeanza mkakati wa kuandaa namna ya uteketezaji wa taka za vifaa vya kielektroniki ikiwa ni pamoja na simu na vifaa vingine kutokana na vifaa hivyo kutengenezwa kwa madini mengi ambayo ni sumu kwenye mazingira 

Rai hiyo imetolewa na Waziri wa Habari Nape Nnauye ambaye amesema Takwimu za  taka sumu zitokanazo na vifaa vya mawasiliano kama  simu, vifaa vya kiteknolojia  ukanda wa Afrika mashariki zinazidi kuongezeka ambapo taka hizo zinaweza kutumika pia kama fursa kutokana na madini yaliyomo.

Hata hivyo Katibu Mkuu wa Taasisi ya mawasiliano ya Afrika mashariki taka za kielektroniki zinakuwa kwa kasi ambapo kwa Tanzania taka hizi hufikia hadi tani elfu 19 kwa Mwaka kuliko taka zingine na kwamba endapo utaratibu utawekwa mzuri taka hizi ni fursa kutokana na wingi wa madini yaliyomo.

Utaratibu wa uzalishaji na udhibiti wa taka hizi umekuwa ukitofautiana na nchi na nchi katika umoja huu wa nchi za Afrika mashariki ambapo kupitia mkutano huu wadau wamekutana kujadili mpango maalum wa udhibiti wa pamoja.

Kwa upande wa mamlaka ya mawasiliano nchini TCRA wamesema lengo kubwa kwa sasa ni kusambaza elimu kwa wadau wote wakiwemo wasimamizi wa mazingira,wananchi na watunga sera.