Alhamisi , 7th Jan , 2016

Mtandao wa watetezi wa haki za binadamu nchini (THRDC), wameyataka mashirika na taasisi za kusaidia jamii, makanisa na misikiti kuwasaidia watu wanaovunjiwa nyumba zao na kuachwa bila makazi.

Mratibu wa mtandao wa watetezi wa haki za binadamu Onesmo Olengurumwa akizungumza na waandishi wa habari

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa taasisi hiyo Onesmo Ole Ngurumwa wakati akiongea na East Africa Radio juu ya zoezi la bomoa bomoa linaloendelea nchi nzima na kuongeza kuwa serikali ilifanya makosa kuacha watu wajenge maeneo hatarishi na yasiyoruhusiwa na hivyo wanawajibika kuwatafutia maeneo mbadala ya kuishi kabla ya kuwavunjia nyumba zao.

Ole Ngurumwa ametahadharisha kuwa watu laki mbili watakaoathirika na zoezi hilo watazalisha wezi na watu wasio na makazi na watoto wengi wa mitaani kitu ambacho ni hatari kwa jamii.

Aidha Onesmo Ole Ngurumwa amesema kuwa Tanzania ina eneo kubwa ambapo serikali ingeweza kuwajengea nyumba za gharama nafuu na kuwahamishia huko kabla ya kuwavunjia kama alivyofanya Rais wa kwanza wa Zanzibar mzee Abeid Karume