Jumatano , 23rd Sep , 2020

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi, (CCM), Kassim Majaliwa, amesema kuwa mgombea urais wa chama hicho Dkt.John Magufuli ni kiongozi anayestahili kupewa nchi kwa sababu ana uwezo wa kuongoza.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa

Ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na wakazi wa kata za Lubuga na Ilungu, wilayani Magu, mkoani Mwanza kwenye mikutano ya kuwanadi wagombea wa CCM iliyofanyika akiwa njiani kuelekea jijini Mwanza.

"Dkt Magufuli ana uwezo wa kupewa nchi kwa sababu suala la kupewa nchi siyo la mzaha, wamejitokeza wengi lakini siku ya kupiga kura ni lazima uwe makini, umpe mtu unayemjua historia yake, Dkt. Magufuli amekuwa waziri kwa miaka 20 ameongoza wizara nyeti na kubwa na amekuwa na uwezo wa kuzisimamia na kuleta maendeleo", amesema Waziri Mkuu. 
 
Aidha Waziri Mkuu ameongeza kuwa, "Tanzania imekosa maendeleo ya haraka kwa sababu kulikuwa na tabia ya watu wachache ya kula rushwa na kuwaathiri wananchi wa chini wasipate mafanikio, tunataka kiongozi wa nchi anayeweza kupambana na rushwa na mafisadi na huyo ndiye kiongozi tunayemtaka".