Alhamisi , 1st Nov , 2018

Mkuu wa Mkoa Tabora, Agrey Mwanri amesema hakumbuki chochote kama alishawahi kumwajibisha, Msemaji wa Klabu ya Simba ya jijini Dar es salaam Haji Manara wakati akiwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa.

Mkuu wa Mkoa wa Tabora Agrey Mwanri.

Akizungumza na www.eatv.tv Mkuu huyo wa Mkoa amesema hawezi kuyasemea madai hayo kwa kile alichokieleza kutokuwa na taarifa yoyote juu ya Haji Manara wakati akiwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Dar es salaam.

Mimi sio mtu wa mitandao na wala sio mtu wa magrupu katika suala hili huwezi amini sijawahi na sikumbuki, na wala sina jibu lolote kwa sababu sina undani wake.” Agrey Mwanri

Aidha Mwanri amezungumzia juu ya kuwafurahisha watu wakati anapokuwa anahutubia na kusema mara nyingi huwa haelewi sababu ya watu kucheka badala yake amependekeza kuulizwa watu ambao wamekuwa wakifurahishwa misemo yake.

Mimi siwezi kujua kama nina kipaji cha kuigiza, ila kimoja ambacho nakifahamu nikisimamia jambo sauti yangu huwa inapanda sana, ndio maana siwezi kulea mtoto mdogo kwa sababu atashikwa napresha ndio maana nikizungumza wakati mwingine huwa naomba msamaha.” Amesema Mwanri

Kuhusiana mimi kuwa na kipaji cha kuigiza huwa sifahamu labda uwaulize watu, lakini kama watu wamefurahishwa na sauti na jinsi navyosukuma mambo namshukuru Mungu."

Mkuu huyo wa Mkoa kwa kushirikiana na wataalamu kwenye mkoa wake na moja ya kampuni ya kitanzania wameandaa jukwaa maalum la kuhamasisha uwekezaji mkoani Tabora lengo likiwa ni kuinua uchumi wa wakazi wa mkoa huo.