Ijumaa , 25th Mar , 2022

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema kwa sasa hatatoa ajira kwa askari wa Jeshi la Magereza na kwamba askari waliopo wanaweza kuwasimamia wafungwa hatakama wana vyeo kwakuwa wanaouzoefu wa kutosha.

Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Rais Samia ameyasema hayo leo Machi 25, 2022 alipokuwa akizinduwa na kuweka jiwe la msingi kwenye miradi ya Jeshi la Magereza Jijini Dodoma.

"Kuhusu kuajiri hatuwezi kuajiri kila mwaka, sitatoa kwa sasa ajira mpya kwasababu bili ya ajira ni kubwa mno. Nimeongea na kamishina akasema nimpatie hata darasa la saba wakasimamie wafungwa, suala la kusimamia wafungwa linahitaji uzoefu" amesema Rais Samia Suluhu.

Katika hatua nyingine, Mhe. Rais Samia amelipongeza Jeshi la Magereza kwa kufanya vizuri kwenye shughuli za uzalishaji mali na kwamba serikali inajivunia uwepo wa Jeshi hilo. Licha ya kuonesha kufurahishwa na miradi ya Jeshi hilo, Rais Samia amelitaka Jeshi hilo kuwa na mahusiano mazuri na wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi kwani amegundua hakuna muunganiko mzuri kati ya jeshi hilo na wizara.

Katika hotuba yake, Rais Samia amezungumzia pia suala la msongamano wa mahabusu na kusema kwamba awali alishaongea na DPP kuona namna ya kuwapunguza mahabusu gerezani ikiwemo kuwaachia mahabusu ambao kesi zao hazina ushahidi na kesi zingine ambazo hazina uzito.

Pia Mhe. Rais Samia amechangia mifuko elfu moja ya saruji ili isaidie kukamilisha jengo la huduma ya mama na mtoto katika hospitali ya kanda ya Jeshi la Magereza, na akasisitiza kuangalia kwenye mifuko mingine ya bajeti kama wanaweza kutia nguvu katika mradi huo ambao ameonekana kuguswa nao.